Thursday, July 17, 2014

Ninasoma Vitabu Vitatu kwa Mpigo

Siku hizi, nimekuwa nikisoma vitabu vitatu kwa mpigo. Kitabu kimojawapo ni A Moveable Feast cha Ernest Hemingway. Hiki ni kati ya vitabu vya Hemingway vilivyochapishwa baada ya kufariki kwake. Mswada wa kitabu hiki ulihaririwa kwanza na Mary Welsh, mke wake wa nne na wa mwisho, ukachapishwa mwaka 1964.

Mimi ninasoma toleo jipya la mswada huu, ulivyohaririwa na Sean Hemingway, na kuandikiwa utangulizi na Patrick Hemingway. Toleo hili lilichapishwa mwaka 2009. Miaka ya 1921 hadi 1926 Hemingway aliishi Paris, na kitabu kinaelezea mambo ya wakati ule, yakiwemo mahusiano yake na waandishi mashuhuri kama Gertrude Stein, ambaye alichangia sana kumkomaza kijana Hemingway katika uandishi. Bado ninakisoma, isipokuwa habari zake nimezifahamu kwa miaka kadhaa.

Kitabu kingine ninachosoma ni Nomad (New York: Free Press, 2011), kilichotungwa na Ayaan Hirsi Ali. Kinahusu maisha yake. Huyu ni mama aliyezaliwa Somalia, akalelewa katika u-Islam. Baadaye aliacha dini hiyo, kitendo ambacho kilisababisha awe mkimbizi, kwani kuacha u-Islam ni kosa kubwa, naye amelazimika kuishi kama mkimbizi Ulaya na sasa Marekani, akihofia kuuawa. Msimamo wa Ayaan Hirsi Ali ni kwamba u-Islam ni dini katili na kandamizi, hasa kwa wanawake. Ayaan anasema hana dini. Binafsi, ningependa watu wakisome kitabu chake, na kama wanaweza kuupinga msimamo wake, tutafaidika sana, hasa sisi ambao si wa-Islam.

Kitabu cha tatu ninachosoma ni The Pearl (New York: Bantam, 1973), kilichotungwa na John Steinbeck, mwandishi maarufu m-Marekani, aliyepata tuzo ya Nobel mwaka 1962. Binafsi,  nisikiapo jina la Steinbeck, nawazia kwanza riwaya zake za The Grapes of Wrath na  Of Mice and Men. Vile vile, jina la Steinbeck linanirudisha kwenye miaka ya sitini na kitu, nilipokuwa nasoma sekondari. Nilisoma riwaya yake ya The Moon is Down, ambayo ilinigusa sana, ikazitawala hisia zangu kwa namna ambayo nashindwa kuelezea.

Huu ni wakati wa likizo. Nina muda mwingi wa kujisomea vitabu ninavyopenda, bila kusukumwa na mahitaji ya shule. Panapo majaliwa, nikishamaliza kusoma vitabu hivi ninavyovisoma wakati huu, nitaviongelea katika blogu hii.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...